WALIMU WA SHULE YA MSINGI ZANZIBAR WAPATIWA MAFUNZO YA ELIMU MTANDAO

Kampuni ya Moyo Media ikishirikiana na Shaibu Foundation na American Corner Pemba kwa kupitia harambee ya “LEARN & DONATE” yaani JIFUNZE na UCHANGIE wameanza kutoa mafunzo kwa vitendo kwa walimu wa shule ya Madungu msingi kisiwani Pemba. Ikiwa ni moja ya njia ya kuwajengea uwezo walimu juu ya utumiaji wa mtandao kama nyenzo ya kufundishia.

Walimu hao walianza kupatiwa elimu maelezo “theory” wiki 2 zilizopita, sasa ni wakati wa kupatiwa elimu kwa vitendo “practical”. Mafunzo yatakapokamilika mwalimu ataweza kutumia mfumo wa kufundishia kwa njia ya mtandao “e-Learning platform” na mwanafunzi ataweza kujifunza n.k kwa kutumia mfumo huo. Hii ni njia ya kisasa zaidi katika sekta ya elimu ambapo nchi zilizoendelea wanatumia kama njia ya kufundisha. Wakati kwa nchi zinazoendelea wanatumia kwa ngazi ya elimu ya juu.

Mafunzo haya ni endelevu na Kampuni ya Moyo Media imepanga kutoa mafunzo haya Tanzania nzima. Kwa shule za Zanzibar, wameanza kutoa mafunzo kwa shule ya Madungu msingi na yatakapokamilika wataendelea kwa shule nyingine.

Lengo la Mafunzo haya:

Ni kuwajengea utamaduni wanajamii kujitolea kwa hiari, pia kusaidia mradi wa ujenzi wa Mskiti unaoendelea wilaya ya Madaba, Mkoa wa Ruvuma, Tanzania.

Kwa mtazamo wa haraka, binadamu tuliowengi hatuna utamaduni wa kujitolea hata kwa miradi ya kijamii. Hivyo Kampuni ya Moyo Media ikishirikiana na Shaibu Foundation wameandaa harambee hii ili kuwafanya wanajamii watambue kuwa unapochangia hupotezi kitu, na kuna faida nyingi zinazotokana na jamii yenyewe na hata kwa Mungu pia, ndio mwanadamu anapopata Baraka zaidi. Maana wahenga walisema “Ni Baraka kutoa, Kuliko KUPOKEA”

CHANZO: Pemba Live